
Wakati wa utafiti wetu Tanzania mnamo mwaka 2019 kwaajili ya mradi wa Mama na Ualbino, tulisikia mara kadhaa kwamba viongozi wa kidini wana ushawishi mkubwa katika jamii katika utoaji wa misaada, elimu na utetezi. Kiongozi mmoja wa kiislam alisema kwamba “viongozi wa kidini tayari wana uwezo wa kufikia sehemu za ndani zaidi za jamii….. wanasikilizwa na kupokelewa na watu. Viongozi hawa ni watengenezaji wa mitazamo. Watu hufuata wasemacho…. Kwahiyo dini hupewa kipaumbele cha kwanza hata kabla ya serikali na siasa”
Kulikua na kikundi cha mipango kilichojumuisha washirika kutoka Tanzania na Canada: Perpetua Senkoro (Mwezeshaji Tafsiri, TZ), Kondo Seif (Mwezeshaji Tafsiri, TZ), Mchungaji Cannon Thomas Godda (Mkurugenzi Mkuu, Baraza la Dini Mbalimbali Kwaajili ya Amani, TZ), Sheryl Reimer-Kirkham (Mkuu wa Mradi, CA), Barbara Astle (Mkuu Msaidizi wa Mradi, CA), Emma Strobell (Meneja Mradi, CA), and Meghann Buyco (Mtafiti Msaidizi, CA).
Tangu Novemba 2021 mpaka Januari 2022, tulifanikiwa kuendesha mikutano ya zoom minne ya viongozi wa dini mbalimbali nchini Tanzania, Perpetua Senkoro akiwa mwezeshaji. Alikua mtu sahihi kuendesha mikutano hii kwasababu yeye mwenyewe ni mwanamke mwenye ualbino na pia ni afisa haki za binadamu. Ilikuwa sahihi pia kwa Kondo Seif, mtu mwenye ualbino, kufundisha kuhusu baiolojia na sababu za kinasaba zinazopelekea hali ya ualbino kutokea.
Jumla ya viongozi wa dini wa Kiislamu na Kikristo 29 wa mkoani Mwanza, Dar es salaam na Shinyanga walihudhuria mikutano hiyo. Aidha, kinamama tisa wa kikundi cha “Upendo wa Mama” walikuwepo pia. Hiki ni kikundi cha kuzalisha kipato cha wamama wenye kuathiriwa na ualbino. Wamama hawa walitoa uzoefu wao kwa viongozi wa dini pamoja na kuwaeleza wasiwasi wao kuhusu ushirikishwaji. Walichangia katika masuala yote mikutanoni hususan katika “tamko la viongozi wa dini”.
Kwenye mikutano hii vinne, viongozi wa Kiislamu na Kikristo pamoja na wamama waliweza kufanya mijadala yenye tija. Mijadala hii ilitokana na maandiko matakatifu pamoja na matendo ya kidini ili kutengeneza hatua bora za kukuza haki za watu wenye ualbino. Kila mkutano ulikua na wawasilishaji wageni pamoja na mijadala ya vikundi kuhusu mada mahususi:
Mkutano #1, Novemba 27, 2021 “Wamama na Ualbino”
Mkutano #2, Desemba 5, 2021 “Nafasi ya Viongozi wa Dini”
Mkutano #3, Januari 8, 2022 “Misingi ya Kidini”
Mkutano #4, Januari 22, 2022 “Hatua za Pamoja”
Kwenye mkutano wa tatu, Marco Methuselah (Seminari ya Theolojia ya Mt.Paul, Mwanza TZ), Sheikh Hassan Kabeke (Mwanza TZ), na Mchungaji Valentine Mbuke (Mwanza TZ) walitoa mawasilisho kuhusu mafundisho ya kiimani pamoja na uzoefu wao katika kutetea haki za watu wenye ualbino. Viongozi wa dini walisisitiza kuhusu miongozo iliyomo katika vitabu vitakatifu (Biblia na Qura’an), wakati wakifundisha kuhusu thamani ya binadamu kama alivyoumbwa na Mungu/Allah. Palikuwepo pia mafundisho mengi dhidi ya ubaguzi na vitendo vyenye kudhuru wengine.

Kwenye mkutano wa nne, Ikponwosa Ero (Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Utetezi wa shirika la Under the Same Sun, Mshauri wa Jukwaa la Ualbino Afrika, na Mtaalamu Huru Mstaafu wa masuala ya ualbino Umoja wa Mataifa) alielezea kuhusu namna mikutano hii inavyokuza haki za watu wenye ualbino. Akirejelea Tamko la Umoja wa Mataifa la Beirut (2017) kuhusu Imani na Haki za Binadamu, Ero aliwaomba viongozi wa dini kutumia kimkakati mamlaka yao ya kimaadili na kiimani katika kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu. Alikazia kwamba mikutano hii na tamko la viongozi wa dini ni mifano thabiti ya kufuatwa na nchi zingine.
Mikutano hii ilitoka na Tamko la Pamoja la Viongozi wa Dini, lililojikita katika kukemea namna zote za unyanyapaa na kuhamasisha amani na upendo kwa watu wenye ualbino. Tamko hili limejumuisha mapendekezo kwa serikali, viongozi wa dini, jamii na watu wenye ualbino. Wawakilishi wawili waliwasilisha tamko hili kwa Serikali ya Tanzania (Ofisi ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu wenye Ulemavu Dodoma) mnamo Februari 7, 2022. Kikao na waandishi wa habari kilifuata tarehe 22 Februari mkoani Mwanza ambapo tamko hilo lilisomwa na kamati ya Amani ya viongozi wa dini wa mkoa wa Mwanza.

Imetafsiriwa na: Perpetua Senkoro
Imeandikwa na:

Perpetua Senkoro (Knowledge Translation Facilitator, TZ)
Reverend Cannon Thomas Godda (Executive Director, Interreligious Council for Peace, TZ)
Kondo Seif (Knowledge Translation Facilitator, TZ)

Meghann Buyco, Graduate Research Assistant

Dr. Sheryl Reimer-Kirkham, Project lead

Emma Strobell, Project Coordinator

Dr. Barbara Astle, Project Co-lead
1 thought on “Mkutano wa Viongozi wa Dini Tanzania”